Description
Hakika mirathi ya Ahlul-Bait ambayo imehifadhiwa na kambi yao na wafuasi wao dhidi ya upotovu inaonyesha kambi iliyokusanya aina mbalimbali za taaluma za kiislamu.
Kambi hii imeweza kulea nafsi mbalimbali zilizotayari kunywa kutoka kwenye chemchemu hiyo, na kuupa umma wa kiislamu wanachuoni wakubwa wenye kufuata nyayo za ujumbe wa Ahlul-Bait.Wanachuoni waliokusanya vidodosa na maswali mbalimbali ya madhehebu na mitazamo tofauti ya kifikira kuanzia ndani ya desturi ya kiislamu hadi nje ya desturi hiyo, huku wao wakitoa majibu na utatuzi makini juu ya maswali hayo ndani ya karne zote.
Jumuiya ya kimataifa ya Ahlul-Bait imefanya hima kutetea utukufu wa ujumbe wa Uislamu na ukweli wake ambao umechafuliwa na makundi, madhehebu na wanaharakati mbalimbali wenye chuki na Uislamu.
Jumuiya imefuata nyayo za Ahlul-Bait na za wafuasi wa kambi yao njema ambayo imefanya hima kujibu madai yenye kuendelea na daima ikajaribu kubaki ndani ya msitari wa mapambano kwa kiwango kinachohitajika ndani ya kila zama .Hakika uzoefu ambao umehifadhiwa ndani ya vitabu vya wanachuoni wa kambi ya Ahlul-Bait katika dhamira hii ni wa aina ya pekee, kwa sababu una hakiba ya kielimu inayotegemea akili na hoja, huku ukijiepusha na matamanio na upendeleo uliokatazwa.
Unazungumza na wasomi na wanafikra wenye fani maalumu, mazungumzo ambayo yanakubalika kiakili na yanapokewa na maumbile yaliyo salama.